Mk. 4:30-41 Swahili Union Version (SUV)

30. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani?

31. Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi,

32. lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake.

33. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia;

34. wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.

35. Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo.

36. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye.

37. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji.

38. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?

39. Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.

40. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?

41. Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Mk. 4