1. Akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari.
2. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake,
3. Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda;
4. ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila.
5. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba;
6. hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka.
7. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda.
8. Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.
9. Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie.
10. Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano.
11. Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,
12. ili wakitazama watazame, wasione;Na wakisikia wasikie, wasielewe;Wasije wakaongoka, na kusamehewa.
13. Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje?