Mk. 15:5-22 Swahili Union Version (SUV)

5. Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.

6. Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye.

7. Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile.

8. Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea.

9. Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi?

10. Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda.

11. Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba.

12. Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi?

13. Wakapiga kelele tena, Msulibishe.

14. Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe.

15. Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe.

16. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima.

17. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani;

18. wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!

19. Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia.

20. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe.

21. Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.

22. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa.

Mk. 15