20. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe.
21. Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.
22. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa.
23. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee.
24. Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini.
25. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha.
26. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI.
27. Na pamoja naye walisulibisha wanyang’anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [
28. Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.]
29. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu,
30. jiponye nafsi yako, ushuke msalabani.
31. Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe.
32. Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea.
33. Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa.
34. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?