15. Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe.
16. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima.
17. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani;
18. wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!
19. Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia.
20. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe.
21. Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.
22. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa.
23. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee.
24. Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini.
25. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha.
26. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI.
27. Na pamoja naye walisulibisha wanyang’anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [