8. Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani.
9. Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;
10. umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.
11. Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara.
12. Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa.
13. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.
14. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.
15. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa;
16. wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu.
17. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.
18. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake.
19. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini.
20. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani.
21. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka.
22. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu.
23. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.