Mk. 11:5-16 Swahili Union Version (SUV)

5. Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda?

6. Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.

7. Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake.

8. Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani.

9. Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;

10. umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.

11. Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara.

12. Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa.

13. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.

14. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.

15. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa;

16. wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu.

Mk. 11