Mk. 11:15-31 Swahili Union Version (SUV)

15. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa;

16. wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu.

17. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.

18. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake.

19. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini.

20. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani.

21. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka.

22. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu.

23. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.

24. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.

25. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [

26. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]

27. Wakafika Yerusalemu tena; hata alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee,

28. wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?

29. Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.

30. Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni.

31. Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini?

Mk. 11