Mk. 10:11-23 Swahili Union Version (SUV)

11. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;

12. na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.

13. Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea.

14. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao.

15. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa.

16. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.

17. Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?

18. Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.

19. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.

20. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.

21. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.

22. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

23. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

Mk. 10