Mk. 1:11-24 Swahili Union Version (SUV)

11. na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

12. Mara Roho akamtoa aende nyikani.

13. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.

14. Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,

15. akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.

16. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.

17. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.

18. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

19. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao.

20. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.

21. Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.

22. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.

23. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti,

24. akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza?

Mk. 1