Mit. 8:18-32 Swahili Union Version (SUV)

18. Utajiri na heshima ziko kwangu,Naam, utajiri udumuo, na haki pia.

19. Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi,Na faida yangu hupita fedha iliyo teule.

20. Natembea katika njia ya haki,Katikati ya mapito ya hukumu.

21. Niwarithishe mali wale wanipendao,Tena nipate kuzijaza hazina zao.

22. BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake,Kabla ya matendo yake ya kale.

23. Nalitukuka tokea milele, tangu awali,Kabla haijawako dunia.

24. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa,Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji.

25. Kabla milima haijawekwa imara,Kabla ya vilima nalizaliwa.

26. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makondeWala chanzo cha mavumbi ya dunia;

27. Alipozithibitisha mbingu nalikuwako;Alipopiga duara katika uso wa bahari;

28. Alipofanya imara mawingu yaliyo juu;Chemchemi za bahari zilipopata nguvu;

29. Alipoipa bahari mpaka wake,Kwamba maji yake yasiasi amri yake;Alipoiagiza misingi ya nchi;

30. Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi;Nikawa furaha yake kila siku;Nikifurahi daima mbele zake;

31. Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu;Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.

32. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa;Maana heri hao wazishikao amri zangu.

Mit. 8