Mit. 30:7-21 Swahili Union Version (SUV)

7. Mambo haya mawili nimekuomba;Usininyime [matatu] kabla sijafa.

8. Uniondolee ubatili na uongo;Usinipe umaskini wala utajiri;Unilishe chakula kilicho kadiri yangu.

9. Nisije nikashiba nikakukana,Nikasema, BWANA ni nani?Wala nisiwe maskini sana nikaiba,Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.

10. Usimchongee mtumwa kwa bwana wake;Asije akakulaani, ukaonekana una hatia.

11. Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao;Wala hawambariki mama yao.

12. Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe;Ambao hawakuoshwa uchafu wao.

13. Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini!Na kope zao zimeinuka sana.

14. Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga;Na vigego vyao ni kama visu.Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu.

15. Mruba anao binti wawili,Waliao, Nipe! Nipe!Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe,Naam, vinne visivyosema, Basi!

16. Kuzimu; na tumbo lisilozaa;Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!

17. Jicho la mtu amdhihakiye babaye,Na kudharau kumtii mamaye;Kunguru wa bondeni wataling’oa,Na vifaranga vya tai watalila.

18. Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu,Naam, kuna manne nisiyoyafahamu.

19. Mwendo wa tai katika hewa;Na mwendo wa nyoka juu ya mwamba;Mwendo wa merikebu katikati ya bahari;Na mwendo wa mtu pamoja na msichana.

20. Hivyo ndivyo mwendo wa mwanamke mzinifu;Hula, akapangusa kinywa chake,Akasema, Sikufanya uovu.

21. Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka,Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia.

Mit. 30