Mit. 3:6-23 Swahili Union Version (SUV)

6. Katika njia zako zote mkiri yeye,Naye atayanyosha mapito yako.

7. Usiwe mwenye hekima machoni pako;Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.

8. Itakuwa afya mwilini pako,Na mafuta mifupani mwako.

9. Mheshimu BWANA kwa mali yako,Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.

10. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi,Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.

11. Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na BWANA,Wala usione ni taabu kurudiwa naye.

12. Kwa kuwa BWANA ampendaye humrudi,Kama vile baba mwanawe ampendezaye.

13. Heri mtu yule aonaye hekima,Na mtu yule apataye ufahamu.

14. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha,Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.

15. Yeye ana thamani kuliko marijani,Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.

16. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume,Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.

17. Njia zake ni njia za kupendeza sana,Na mapito yake yote ni amani.

18. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana;Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.

19. Kwa hekima BWANA aliiweka misingi ya nchi;Kwa akili zake akazifanya mbingu imara;

20. Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika;Na mawingu yadondoza umande.

21. Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako,Shika hekima kamili na busara.

22. Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako,Na neema shingoni mwako.

23. Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama,Wala mguu wako hautakwaa.

Mit. 3