1. Mwanangu, usiisahau sheria yangu,Bali moyo wako uzishike amri zangu.
2. Maana zitakuongezea wingi wa siku.Na miaka ya uzima, na amani.
3. Rehema na kweli zisifarakane nawe;Zifunge shingoni mwako;Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.
4. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri,Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.
5. Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote,Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6. Katika njia zako zote mkiri yeye,Naye atayanyosha mapito yako.
7. Usiwe mwenye hekima machoni pako;Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.
8. Itakuwa afya mwilini pako,Na mafuta mifupani mwako.
9. Mheshimu BWANA kwa mali yako,Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi,Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.
11. Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na BWANA,Wala usione ni taabu kurudiwa naye.
12. Kwa kuwa BWANA ampendaye humrudi,Kama vile baba mwanawe ampendezaye.
13. Heri mtu yule aonaye hekima,Na mtu yule apataye ufahamu.
14. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha,Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.
15. Yeye ana thamani kuliko marijani,Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.
16. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume,Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.
17. Njia zake ni njia za kupendeza sana,Na mapito yake yote ni amani.
18. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana;Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.