Mit. 29:8-22 Swahili Union Version (SUV)

8. Watu wenye dharau huwasha mji moto;Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu.

9. Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu;Akikasirika au akicheka, pia hapana raha.

10. Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu;Bali wenye haki humtunza nafsi yake.

11. Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote;Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.

12. Mwenye kutawala akisikiliza uongo;Basi watumishi wake wote watakuwa waovu.

13. Maskini na mdhalimu hukutana pamoja;BWANA huwatia nuru macho yao wote wawili.

14. Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu;Kiti chake cha enzi kitathibitika milele.

15. Fimbo na maonyo hutia hekima;Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.

16. Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka;Bali wenye haki watayatazama maanguko yao.

17. Mrudi mwanao naye atakustarehesha;Naam, atakufurahisha nafsi yako.

18. Pasipo maono, watu huacha kujizuia;Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.

19. Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno;Maana ajapoyafahamu hataitika.

20. Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno?Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.

21. Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto,Mwisho wake atakuwa ni mwanawe.

22. Mtu wa hasira huchochea ugomvi;Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.

Mit. 29