Mit. 29:3-12 Swahili Union Version (SUV)

3. Apendaye hekima humfurahisha babaye;Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali.

4. Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu;Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

5. Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake,Hutandika wavu ili kuitega miguu yake.

6. Kuna mtego katika kosa la mtu mbaya;Bali mwenye haki huimba na kufurahi.

7. Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini;Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue.

8. Watu wenye dharau huwasha mji moto;Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu.

9. Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu;Akikasirika au akicheka, pia hapana raha.

10. Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu;Bali wenye haki humtunza nafsi yake.

11. Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote;Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.

12. Mwenye kutawala akisikiliza uongo;Basi watumishi wake wote watakuwa waovu.

Mit. 29