Mit. 29:15-27 Swahili Union Version (SUV)

15. Fimbo na maonyo hutia hekima;Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.

16. Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka;Bali wenye haki watayatazama maanguko yao.

17. Mrudi mwanao naye atakustarehesha;Naam, atakufurahisha nafsi yako.

18. Pasipo maono, watu huacha kujizuia;Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.

19. Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno;Maana ajapoyafahamu hataitika.

20. Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno?Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.

21. Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto,Mwisho wake atakuwa ni mwanawe.

22. Mtu wa hasira huchochea ugomvi;Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.

23. Kiburi cha mtu kitamshusha;Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.

24. Mshiriki wa mwivi huichukia nafsi yake mwenyewe;Asikia maapizo, wala hana neno.

25. Kuwaogopa wanadamu huleta mtego;Bali amtumainiye BWANA atakuwa salama.

26. Watu wengi hutafuta upendeleo wa mkuu;Bali hukumu ya kila mtu hutoka kwa BWANA

27. Mtu aliye dhalimu ni chukizo kwa wenye haki;Na mnyofu wa mwenendo ni chukizo kwa waovu.

Mit. 29