Mit. 28:3-18 Swahili Union Version (SUV)

3. Mtu mhitaji awaoneaye maskini,Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.

4. Wao waiachao sheria huwasifu waovu;Bali wao waishikao hushindana nao.

5. Watu wabaya hawaelewi na hukumu;Bali wamtafutao BWANA huelewa na yote.

6. Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake,Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.

7. Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima;Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.

8. Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida,Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.

9. Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria,Hata sala yake ni chukizo.

10. Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya,Ataanguka katika rima lake mwenyewe;Bali wakamilifu watarithi mema.

11. Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe;Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.

12. Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi;Bali waovu waondokapo, watu hujificha.

13. Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

14. Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote;Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.

15. Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa;Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.

16. Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana;Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.

17. Aliyelemewa na damu ya mtuAtalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.

18. Aendaye kwa unyofu ataokolewa;Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.

Mit. 28