15. Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa;Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.
16. Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana;Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.
17. Aliyelemewa na damu ya mtuAtalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.
18. Aendaye kwa unyofu ataokolewa;Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.
19. Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele;Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.
20. Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele;Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.
21. Kupendelea watu si kwema;Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.
22. Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri;Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.
23. Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali;Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.
24. Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa;Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.
25. Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina;Bali amtumainiye BWANA atawandishwa.
26. Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga;Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.
27. Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu;Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.