Mit. 27:7-19 Swahili Union Version (SUV)

7. Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali;Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.

8. Kama ndege aendaye huko na huko mbali na kitundu chake;Ndivyo alivyo mtu aendaye huko na huko mbali na mahali pake.

9. Marhamu na manukato huufurahisha moyo;Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake.

10. Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako,Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako.Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.

11. Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu;Ili nipate kumjibu anilaumuye.

12. Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha;Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.

13. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni;Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya.

14. Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema;Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.

15. Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi,Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;

16. Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo;Na mkono wake wa kuume hukuta mafuta.

17. Chuma hunoa chuma;Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.

18. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake;Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.

19. Kama uso ufananavyo na uso katika maji;Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake.

Mit. 27