1. Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda, walizinakili.
2. Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo;Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.
3. Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini;Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki.
4. Ondoa takataka katika fedha,Na chombo kitatokea kwa mtakasaji;
5. Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme,Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki.
6. Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme;Wala usisimame mahali pa watu wakuu;
7. Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele;Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu.Yale uliyoyaona kwa macho,
8. Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania;Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye,Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha.
9. Ujitetee na mwenzako peke yake;Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;
10. Yeye asikiaye asije akakutukana;Na aibu yako isiondoke.
11. Neno linenwalo wakati wa kufaa,Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.
12. Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi;Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo.
13. Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno;Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao;Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao.
14. Kama mawingu na upepo pasipo mvua;Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo.
15. Kwa uvumilivu mwingi mkuu husadikishwa;Na ulimi laini huvunja mfupa.