Mit. 24:7-22 Swahili Union Version (SUV)

7. Kwa mpumbavu hekima haipatikani;Hafumbui kinywa chake langoni.

8. Mtu afikiriye kutenda maovu,Watu watamwita mtundu;

9. Fikira za mpumbavu ni dhambi,Na mwenye mzaha huwachukiza watu.

10. Ukizimia siku ya taabu,Nguvu zako ni chache.

11. Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe;Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe.

12. Ukisema, Sisi hatukujua hayo;Je! Yeye aipimaye mioyo siye afahamuye?Naye ailindaye nafsi yako siye ajuaye?Je! Hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake?

13. Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema,Na sega la asali lililo tamu ulionjapo.

14. Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako;Ikiwa umekwisha kuiona;Ndipo itakapofuata thawabu;Wala tumaini lako halitabatilika.

15. Ewe mtu mbaya, usiyavizie makao yake mwenye haki;Wala usipaharibu mahali pake pa kupumzika;

16. Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena;Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.

17. Usifurahi, adui yako aangukapo;Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

18. BWANA asije akaliona hilo, likamkasirisha;Akageuzia mbali naye hasira yake.

19. Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya;Wala usiwahusudu wabaya;

20. Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu;Taa ya mtu mbaya itazimika.

21. Mwanangu, mche BWANA, na mfalme;Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;

22. Maana msiba wao utatokea kwa ghafula;Tena ni nani aujuaye uharibifu wa miaka yao.

Mit. 24