Mit. 24:16-30 Swahili Union Version (SUV)

16. Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena;Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.

17. Usifurahi, adui yako aangukapo;Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

18. BWANA asije akaliona hilo, likamkasirisha;Akageuzia mbali naye hasira yake.

19. Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya;Wala usiwahusudu wabaya;

20. Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu;Taa ya mtu mbaya itazimika.

21. Mwanangu, mche BWANA, na mfalme;Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;

22. Maana msiba wao utatokea kwa ghafula;Tena ni nani aujuaye uharibifu wa miaka yao.

23. Haya nayo pia ni maneno ya wenye akili.Kupendelea watu katika hukumu si kwema.

24. Amwambiaye mtu mwovu, Wewe una haki;Kabila za watu watamlaani, taifa watamchukia.

25. Bali kwao wakemeao furaha itakuwako;Na baraka ya kufanikiwa itawajilia.

26. Aibusu midomo atoaye jawabu la haki.

27. Tengeneza kazi yako huko nje,Jifanyizie kazi yako tayari shambani,Ukiisha, jenga nyumba yako.

28. Usimshuhudie jirani yako pasipo sababu,Wala usidanganye kwa midomo yako.

29. Usiseme, Nitamtenda kama alivyonitenda mimi;Nitamlipa mtu huyo sawasawa na tendo lake.

30. Nalipita karibu na shamba la mvivu,Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.

Mit. 24