Mit. 20:11-29 Swahili Union Version (SUV)

11. Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake;Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili.

12. Sikio lisikialo, na jicho lionalo,BWANA ndiye aliyeyafanya yote mawili.

13. Usipende usingizi usije ukawa maskini;Fumbua macho yako nawe utashiba chakula.

14. Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi;Lakini akiisha kwenda zake hujisifu.

15. Dhahabu iko, na marijani tele;Lakini midomo ya maarifa ni kito cha thamani.

16. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni;Mtoze rehani aliye mdhamini wa wageni.

17. Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu;Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe.

18. Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana;Na kwa shauri la akili fanya vita.

19. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri;Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana.

20. Amlaaniye babaye au mamaye,Taa yake itazimika katika giza kuu.

21. Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka,Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa.

22. Usiseme, Mimi nitalipa mabaya;Mngojee BWANA, naye atakuokoa.

23. Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa BWANA;Tena mizani ya hila si njema.

24. Mwenendo wa mtu watoka kwa BWANA;Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake?

25. Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu;Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari.

26. Mfalme mwenye hekima huwapepeta wasio haki;Naye hulipitisha gurudumo la kupuria juu yao.

27. Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA;Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake.

28. Fadhili na uaminifu humhifadhi mfalme,Na kiti chake cha enzi huthibitishwa kwa fadhili.

29. Fahari ya vijana ni nguvu zao,Na uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi.

Mit. 20