1. Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake,Kuliko mpotofu wa midomo aliye mpumbavu.
2. Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa;Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi.
3. Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake;Na moyo wake hununa juu ya BWANA.
4. Utajiri huongeza rafiki wengi;Bali maskini hutengwa na rafiki yake.
5. Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa;Wala asemaye uongo hataokoka.
6. Watu wengi watamsihi mkuu ili awafadhili;Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu.
7. Ndugu zote wa maskini humchukia;Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye!Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka.
8. Apataye hekima hujipenda nafsi yake;Ashikaye ufahamu atapata mema.
9. Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa;Naye asemaye uongo ataangamia.