Mit. 18:9-23 Swahili Union Version (SUV)

9. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake,Ni ndugu yake aliye mharabu.

10. Jina la BWANA ni ngome imara;Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.

11. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu;Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake.

12. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna;Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

13. Yeye ajibuye kabla hajasikia,Ni upumbavu na aibu kwake.

14. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake;Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?

15. Moyo wa mwenye busara hupata maarifa;Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa.

16. Zawadi ya mtu humpatia nafasi;Humleta mbele ya watu wakuu.

17. Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki;Lakini jirani yake huja na kumchunguza.

18. Kura hukomesha mashindano;Hukata maneno ya wakuu.

19. Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu;Na mashindano ni kama mapingo ya ngome.

20. Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake;Atashiba mazao ya midomo yake.

21. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi;Na wao waupendao watakula matunda yake.

22. Apataye mke apata kitu chema;Naye ajipatia kibali kwa BWANA.

23. Maskini hutumia maombi;Bali tajiri hujibu kwa ukali.

Mit. 18