Mit. 17:1-13 Swahili Union Version (SUV)

1. Afadhali mego kavu pamoja na utulivu,Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.

2. Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu;Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.

3. Kalibuni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu;Bali BWANA huijaribu mioyo.

4. Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu;Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara.

5. Amdhihakiye maskini humsuta Muumba wake;Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu.

6. Wana wa wana ndio taji ya wazee,Na utukufu wa watoto ni baba zao.

7. Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu;Siuze midomo ya uongo kinywani mwa mkuu.

8. Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho;Kila kigeukapo hufanikiwa.

9. Afunikaye kosa hutafuta kupendwa;Bali yeye akashifuye neno hutenga rafiki.

10. Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu,Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu.

11. Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu;Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake.

12. Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake,Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake.

13. Yeye arudishaye mabaya badala ya mema,Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.

Mit. 17