7. Njia za mtu zikimpendeza BWANA,Hata adui zake huwapatanisha naye.
8. Afadhali mali kidogo pamoja na haki,Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
9. Moyo wa mtu huifikiri njia yake;Bali BWANA huziongoza hatua zake.
10. Kukata maneno huwa katika midomo ya mfalme;Kinywa chake hakitakosa katika hukumu.
11. Mizani ya haki na vitanga vyake ni vya BWANA;Mawe yote ya mfukoni ni kazi yake.
12. Wafalme wakitenda yasiyo haki ni chukizo;Maana kiti cha enzi huthibitika kwa haki.
13. Midomo ya haki ni furaha ya wafalme;Nao humpenda yeye asemaye yaliyo sawa.
14. Hasira ya mfalme ni kama wajumbe wa mauti;Lakini mtu mwenye hekima ataituliza.
15. Kuna uhai katika nuru ya uso wa mfalme,Na fadhili zake ni kama wingu la masika.
16. Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu?Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha.
17. Njia kuu ya mwenye haki ni kujitenga na uovu;Yeye ashikaye njia yake huihifadhi nafsi yake.
18. Kiburi hutangulia uangamivu;Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.
19. Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini,Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi.
20. Atakayelitafakari neno atapata mema;Na kila amwaminiye BWANA ana heri.
21. Aliye na hekima moyoni ataitwa mwenye busara;Utamu wa maneno huongeza elimu.
22. Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao;Bali kufundishwa kwa wapumbavu ni upuzi wao.
23. Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake;Huzidisha elimu ya midomo yake.