1. Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu;Bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA.
2. Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe;Bali BWANA huzipima roho za watu.
3. Mkabidhi BWANA kazi zako,Na mawazo yako yatathibitika.
4. BWANA amefanya kila kitu kwa kusudi lake;Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.
5. Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa BWANA;Hakika, hatakosa adhabu.
6. Kwa rehema na kweli uovu husafishwa;Kwa kumcha BWANA watu hujiepusha na maovu.
7. Njia za mtu zikimpendeza BWANA,Hata adui zake huwapatanisha naye.
8. Afadhali mali kidogo pamoja na haki,Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
9. Moyo wa mtu huifikiri njia yake;Bali BWANA huziongoza hatua zake.