Mit. 13:3-12 Swahili Union Version (SUV)

3. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake;Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.

4. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu;Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.

5. Mwenye haki huchukia kusema uongo;Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.

6. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake;Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.

7. Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu;Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.

8. Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake;Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote.

9. Nuru ya mwenye haki yang’aa sana;Bali taa ya mtu mbaya itazimika.

10. Kiburi huleta mashindano tu;Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.

11. Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka;Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.

12. Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua.Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.

Mit. 13