1. Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.
2. Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu;
3. kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili.
4. Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari;
5. mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia.
6. Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao.