1. Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye amemhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo.
2. Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.
3. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli.
4. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za BWANA, kwa enzi ya jina la BWANA, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.
5. Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtaondokesha wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.
6. Nao wataiharibu nchi ya Ashuru kwa upanga, na nchi ya Nimrodi katika malango yake; naye atatuokoa na Mwashuri, atakapoingia katika nchi yetu, na kukanyaga ndani ya mipaka yetu.