1. Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri;Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.
2. Heri kuiendea nyumba ya matanga,Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake.
3. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko,Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo.
4. Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha.
5. Heri kusikia laumu ya wenye hekima,Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu;
6. Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria,Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu.Hayo nayo ni ubatili.
7. Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima,Na rushwa huuharibu ufahamu.
8. Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake,Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.
9. Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako,Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.