1. Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri;Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.
2. Heri kuiendea nyumba ya matanga,Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake.
3. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko,Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo.
4. Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha.
5. Heri kusikia laumu ya wenye hekima,Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu;
6. Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria,Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu.Hayo nayo ni ubatili.
7. Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima,Na rushwa huuharibu ufahamu.
8. Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake,Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.
9. Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako,Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.
10. Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi?Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo.
11. Hekima ni njema, mfano wa urithi;Naam, nayo ni bora kwao walionao jua.
12. Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.
13. Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?
14. Siku ya kufanikiwa ufurahi,Na siku ya mabaya ufikiri. Mungu ameifanya hiyo moja kwenda sambamba na hiyo ya pili, ili mwanadamu asipate kulijua neno lo lote litakalofuata baada yake.