Mhu. 5:3-16 Swahili Union Version (SUV)

3. Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno.

4. Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri.

5. Ni afadhali usiweke nadhiri,Kuliko kuiweka usiiondoe.

6. Usikiache kinywa chako kuukosesha mwili wako; wala usiseme mbele ya huyo malaika ya kwamba umepitiliwa; kwani Mungu akukasirikie sauti yako, na kuiharibu kazi ya mikono yako?

7. Maana ndivyo ilivyo katika habari za wingi wa ndoto, na ubatili, na maneno mengi; walakini wewe umche Mungu.

8. Ujapokuwa unaona maskini kuonewa, na hukumu na haki kuondolewa kwa jeuri katika jimbo, usilistaajabie jambo hilo; kwa sababu,Aliye juu kuliko walio juu huangalia;Tena wako walio juu kupita hao.

9. Lakini, pamoja na hayo, manufaa ya nchi kwa kila njia ni mfalme anayejibidiisha kwa ajili ya shamba.

10. Apendaye fedha hatashiba fedha,Wala apendaye wingi hatashiba nyongeza.Hayo pia ni ubatili.

11. Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu?

12. Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi.

13. Kuna na balaa mbaya sana niliyoiona chini ya jua, nayo ni hii, mali alizoziweka mwenyewe kwa kujinyima;

14. na mali hizo zimepotea kwa bahati mbaya; naye akiwa amezaa mwana, hamna kitu mkononi mwake.

15. Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake.

16. Hiyo ndiyo balaa mbaya sana, ya kwamba kama vile alivyokuja, vivyo hivyo atakwenda zake; naye amefaidiwa nini mwenye kujitaabisha kwa ajili ya upepo?

Mhu. 5