5. Naam, wataogopa kilichoinukaNa vitisho vitakuwapo njiani;Na mlozi utachanua maua;Na panzi atakuwa ni mzigo mzito;Na pilipili hoho itapasuka;Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele,Nao waombolezao wazunguka njiani.
6. Kabla haijakatika kamba ya fedha;Au kuvunjwa bakuli la dhahabu;Au mtungi kuvunjika kisimani;Au gurudumu kuvunjika birikani;
7. Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa,Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.
8. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!
9. Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.
10. Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli.
11. Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja.
12. Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.
13. Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa;Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.
14. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.