21. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?
22. Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo.
23. Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue;
24. lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua.
25. Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu.
26. Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi.