24. Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo.
25. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.
26. Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.
27. Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,
28. akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.
29. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.
30. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti.
31. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.
32. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.
33. Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.
34. Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo,
35. akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa.
36. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu.
37. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika.
38. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa,
39. lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.