Mdo 28:2-16 Swahili Union Version (SUV)

2. Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida. Kwa maana waliwasha moto, wakatukaribisha sote, kwa sababu ya mvua iliyonyesha na kwa sababu ya baridi.

3. Paulo alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili ya ule moto akamzonga-zonga mkononi.

4. Wenyeji walipomwona yule nyoka akilewa-lewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi.

5. Lakini yeye akamtukusia motoni asipate madhara.

6. Wao wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafula; na wakiisha kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lo lote, wakageuka, wakasema kwamba yeye ni mungu.

7. Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya mkuu wa kisiwa, jina lake Publio; mtu huyu akatukaribisha kwa moyo wa urafiki, akatufanya wageni wake kwa muda wa siku tatu.

8. Ikawa babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza.

9. Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakapozwa;

10. nao wakatuheshimu kwa heshima nyingi; basi tulipoabiri wakatupakilia vitu vile tulivyokuwa na haja navyo.

11. Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha.

12. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu.

13. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli.

14. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi.

15. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka.

16. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.

Mdo 28