12. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini-mashariki na kusini-mashariki.
13. Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang’oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani.
14. Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo,
15. merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa.
16. Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida.
17. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi.
18. Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini.
19. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe.
20. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.
21. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung’oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii.
22. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu.
23. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami,
24. akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe.
25. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.
26. Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja.
27. Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huko na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu.
28. Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano.
29. Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche.
30. Na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu, wakiishusha mashua baharini kana kwamba wanataka kutupa nanga za omo,
31. Paulo akawaambia akida na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka.