13. Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu arobaini.
14. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo.
15. Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia.
16. Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari.
17. Paulo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu.
18. Basi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia.
19. Yule jemadari akamshika mkono akajitenga pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu?
20. Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi.
21. Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hata watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakiitazamia ahadi kwako.
22. Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniarifu haya.
23. Akawaita maakida wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kwa saa tatu ya usiku.
24. Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali.
25. Akaandika barua, kwa namna hii,
26. Klaudio Lisia kwa liwali mtukufu Feliki, Salamu!
27. Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi, wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni Mrumi.
28. Nami nikitaka kulijua lile neno walilomshitakia, nikamtelemsha nikamweka mbele ya baraza;
29. nikaona kwamba ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lo lote la kustahili kuuawa wala kufungwa.
30. Hata nilipopewa habari kwamba patakuwa na vitimvi juu ya mtu huyu, mara nikampeleka kwako, nikawaagiza na wale waliomshitaki, wanene habari zake mbele yako. Wasalamu.
31. Basi, wale askari wakamchukua Paulo kama walivyoamriwa, wakampeleka hata Antipatri usiku;