Mdo 21:3-20 Swahili Union Version (SUV)

3. Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake.

4. Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu.

5. Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba;

6. na baada ya kuagana tukapanda merikebuni, nao wakarudi kwao.

7. Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja.

8. Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake.

9. Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.

10. Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.

11. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.

12. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.

13. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.

14. Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.

15. Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu.

16. Baadhi ya wanafunzi wa Kaisaria wakafuatana na sisi, wakamchukua na Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani ambaye ndiye tutakayekaa kwake.

17. Tulipofika Yerusalemu wale ndugu wakatukaribisha kwa furaha.

18. Hata siku ya pili yake Paulo akaingia kwa Yakobo pamoja nasi, na wazee wote walikuwako.

19. Na baada ya kuwaamkua, akawaeleza mambo yote moja moja Mungu aliyoyatenda katika Mataifa kwa huduma yake.

20. Nao waliposikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia, Ndugu yetu, unaona jinsi Wayahudi walioamini walivyo elfu nyingi, nao wote wana wivu sana kwa ajili ya torati.

Mdo 21