1. Kishindo kile kilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia.
2. Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Uyunani.
3. Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia.
4. Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberoya, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia.
5. Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa.
6. Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.
7. Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.