4. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.
5. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
6. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.
7. Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.
8. Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu.
9. Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano.
10. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani.
11. Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;
12. hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.
13. Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo.
14. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo.