Mdo 18:8-23 Swahili Union Version (SUV)

8. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.

9. Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze,

10. kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu.

11. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu.

12. Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu,

13. wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.

14. Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi;

15. bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo.

16. Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu.

17. Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu.

18. Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu; na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.

19. Wakafika Efeso, akawaacha huko. Yeye mwenyewe akaingia katika sinagogi, akahojiana na Wayahudi.

20. Walipomtaka akae wakati mwingi zaidi, hakukubali;

21. bali aliagana nao, akisema, Nitarejea kwenu tena, Mungu akinijalia. Akatweka, akatoka Efeso,

22. na alipokwisha kushuka Kaisaria, akapanda juu, akawasalimu kanisa, kisha akatelemkia Antiokia.

23. Hata akiisha kukaa huko siku kadha wa kadha akaondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwathibitisha wanafunzi.

Mdo 18