6. Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung’uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa.
7. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi.
8. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.
9. Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze,
10. kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu.
11. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu.
12. Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu,
13. wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.