7. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,
8. wakapita Misia wakatelemkia Troa.
9. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.
10. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.
11. Basi tukang’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli;
12. na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha.
13. Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.
14. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.
15. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.
16. Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.
17. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.