19. Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;
20. wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;
21. tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.
22. Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.
23. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.
24. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale.
25. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.
26. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.
27. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.
28. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.
29. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila;