10. akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.
11. Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.
12. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.
13. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng’ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano.
14. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,
15. wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;
16. ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe.
17. Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha.
18. Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shida, wasiwatolee dhabihu.
19. Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa.
20. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe.
21. Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia,
22. wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.