10. akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?
11. Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.
12. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.
13. Kisha Paulo na wenziwe wakang’oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu.
14. Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi.
15. Kisha, baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa, lisemeni.
16. Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni.
17. Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza.
18. Na kwa muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa.
19. Na alipokwisha kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini;
20. baada ya hayo akawapa waamuzi hata zamani za nabii Samweli.
21. Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini.
22. Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.
23. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;
24. Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake.